Habari na karibu tujijenge!
Maisha yana mambo mengi ndani yake na kimsingi ndizo shughuli ambazo zinaunda ratiba yako ya kila siku. Miongoni mwa mambo haya, mengine ni michakato endelevu na mengine ni mapya yaani huanza na pengine kuisha ndani ya siku husika.
Kama mtu makini, hutakuwa kama mpumbavu na kufanya mambo yako ukianzia msingi mbovu na kutarajia mwenendo au uimara wa jambo ulifanyalo. Kwa maana hio utakuwa makini katika kila hatua ukihakikisha ulifanyalo leo ndio nguvu, nguzo, mwamba, msaada wa shughuli nyingine za kesho.
Hebu fikiri kwa mfano; kama ungetegea kujifunza kuhesabu ukiwa madarasa ya awali na darasa la kwanza, leo ungeweza kuhesabu pesa katika biashara yako? Au kama hukumpenda wala kutaka kumsikiliza mwalimu wa mwandiko akikupiga vidole ukaze mkono na ushike vizuri kalamu, leo hii umefika chuo utaandika tena visivyoeleweka ashindwe kusoma hata mkufunzi wako anayekufunda kuwa mjenzi bora wa taifa lako! Nani ana ajiri asiyejua kusoma au kuandika vizuri au nani aliyefanya biashara vizuri pasipo kujua kuhesabu?
“thamini msingi kwa ngome imara"
Fuata utaratibu, Jenga leo!
Anza na msingi wa mawe juu ya mwamba zisitetemeshwe na kudondosha ukuta, kisha weka vyema kuta za nyumba uijengayo ziwe imara hata kuhimili uzito wa paa na kasi ya upepo, na ukiezeka vizuri pepo zisije vuma na kuezua paa lako.
Nakusihi leo, maisha hayajaisha ungali bado hai, kubali mchakato, kubali kujenga; tofali baada ya tofali zingatia hatua, usirukie nyingine ukiacha nyingine.
Jenga maisha na uishi maisha yenye uthamani.
Na. Mr. Nathanael J. Kiyuga
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni